Saratani ya tumbo ni tatizo linalotishia maisha ya watu kama zilivyo aina nyingine za kansa. Wataalamu wanasema kwamba katika nchi ambayo vyakula vya kila siku vya watu ni vile vilivyohifadhiwa kwa madawa (preservatives), vyenye chumvi (nyingi) na vilivyosindikwa (Pickled foods), idadi ya watu wenye ugongwa wa salatani ya tumbo huwa ni kubwa.
Ukweli wa jambo hilo uko wazi zaidi katika nchi za Asia Mashariki, ambayo wananchi wake wanatumia zaidi vyakula vya aina niliyoitaja hapo juu. Kwa mujibu wa taarifa za mwaka 2008, kansa ya tumbo ndiyo iliyokuwa inaongoza kwa kuua watu wengi zaidi ikilinganishwa na aina nyingine za kansa. Hata hivyo, wataalamu hao wanasema kuwa, katika miaka 25 iliyopita, ugonjwa wa kansa ya tumbo duniani umepungua kwa asilimia sitini (60%). Hii ni kwa sababu ya teknolojia ya kuhifadhi vyakula kwenye majokofu (refrigeration). Vyakula vikihifadhiwa kwenye majokofu (ubaridi) huweza kukaa siku nyingi bila ya kuharibika. Kwa hiyo, mahitaji ya kuhifadhi vyakula kwa kutumia njia zenye kusababisha kansa (kama njia ya kuweka madawa, chumvi, moshi, n.k.) yanapungua.
Ili kupunguza uwezekano wa kupata kansa ya tumbo hasa inayosababishwa na vyakula tunavyokula, watu lazima wazingatie ushauri wa lishe ufuatao:
Kwanza, watu waache kula vyakula vilivyohifadhiwa kwa kutumia madawa hasa ‘nitrites’ na ‘nitrates’. Katika utumbo wa mwanaadamu, madawa hayo yanapambana na vitu vingine vijulikanavyo kama ‘aminesi’. Kutokana na mapambano hayo vitu vyenye kusababisha kansa hutokea. Vitu hivyo vinaitwa ‘nitrosamines’. Siku hizi ni jambo jepesi kununua vyakula visivyokuwa na ‘nitrites’, ‘nitrates’ na madawa mengine ya hatari.
Jambo la kufanya ni kusoma ‘lebo’ kabla ya kununua chakula chochote kilichotengenezwa (kiwandani).
Pili, epuka vyakula vyote vilivyohidhiwa kwa kutumia chumvi na kukaushwa kwa moshi kama vile sausage. Vile vile epuka kula mara kwa mara aina ya vyakula vijulikanavyo kama ‘pickled foods’.
Tatu, watu waepuke kula kila siku vyakula vilivyokaangwa kwa mafuta au vile vilivyookwa kwa kutumia oven (grilled foods). Hii ni kwa sababu njia hizo za kutayarisha vyakula zinasababisha nyama na samaki kutoa vitu vinavyosababisha kansa ya tumbo. Hivyo basi, ni vema watu wakapendelea vyakula vya asili na vile vilivyopikwa au kuokwa kwa njia ambazo si za hatari. Nne, watu wajitahidi kula vyakula vyenye vitamini A, B na C na pia vyenye madini ya ‘selenium’. Kwa ushahidi wa utafiti, vitu hivyo (vitamini na madini) vinasaidia kuzuia kutokea kwa kansa.
Follow Us Here