Mashangingi yaitafuna serikali Tanzania
*Yatumia Sh33bilioni kwa mwaka
Na Ramadhan Semtawa
WAKATI matumizi ya Serikali yakiwa yamezidi bajeti kwa Sh 900 bilioni, imebainika gharama kubwa za kuendesha magari ya kifahari maarufu kama mashangingi ni moja ya chanzo kinachochangia hali hiyo.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kwamba, mashangingi yanayotumiwa na viongozi wa serikali yapo 800 yanatumia zaidi ya Sh33 bilioni kwa mwaka ikiwa ni matumizi ya mafuta na gharama za kuyafanyia mategenezo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana, magari hayo yanatumia wastani wa lita 300 kila moja kwa wiki, hivyo hutumia lita za mafuta 240,000 kwa kipindi hicho kwa magari yote hayo. Kwa wastani bei ya sasa ya mafuta ya diseli ni sh 1200 kwa lita hivyo magari hayo yanatumia Sh1.152 bilioni kwa mwezi. Uchunguzi umegundua kuwa gharama za kulifanyia mategenezo kwa mwezi ni Sh2 milioni kila gari hivyo gharama za kuhudumia magari hayo kwa mwezi ni Sh1.6 bilioni.
Ukijumlisha gharama za mafuta na mategenezo kwa mwezi ni Sh 2.752 bilioni na kwa mwaka ni kiasi cha Sh33 bilioni. Kiasi hicho cha matumizi kingepungua iwapo baadhi ya viongozi ukiachia rais, waziri mkuu na makamu wa rais wangetumia magari ya kawaida.
Kati ya magari hayo, 540 ni ya viongozi wa Serikali Kuu wakiwamo ofisi ya rais, ofisi ya waziri mkuu, makamu wa rais, mawaziri, manaibu mawaziri, makatibu wakuu. Orodha hiyo ya serikali kuu imezingatia, makatibu wakuu 27, manaibu wao 27, maafisa utumishi (Ma Dap) 27, na wakurugenzi wanne kila wizara na sehemu nyingine wakurugenzi wasaidizi, huku Ikulu, ofisi ya makamu wa rais na ya waziri mkuu, kwa pamoja zikiwa na magri hayo yasiyopungua 40.
Mengine hutumiwa na watendaji wakuu wa mashirika na taasisi za serikali, wakati kwa upande wa Tamisemi ni kuanzia wakuu wa mikoa 22, makatibu tawala wa mikoa 22, makatibu tawala wa wilaya, wakurugenzi watendaji wa wilaya na wakuu wa wilaya 104.
Wakati gharama hizo zikionekana kuwa mzigo kwa walipa kodi, Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, ameliambia Mwananchi: "Tena naomba uninukuu vizuri, mawaziri wataendelea kutumia magari yanayoendana na hadhi yao, waziri hawezi kutembelea Vokswagen (Bito)".
Uchunguzi umebaini kuwa gharama hizo zimekuwa zikiongezeka maradufu katika siku za hivi karibuni kutokana mawaziri, manaibu mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wilaya kutotulia ofisini kutokana na ziara wanazofanya katika maeneo mbalimali.
Pia imebainika kwamba, gharama za kuendesha magari hayo zimekuwa ni mzigo kwa walipa kodi kutokana na baadhi ya mawaziri kutofanya kazi vizuri huku baadhi ya magari yakionekana kuranda randa kwenye mabaa nyakati za usiku na mwisho wa wiki. Akizungumzia zaidi kuhusu magari hayo, Chenge alisema serikali haijafikia uamuzi wowote wa kupiga marufuku magari hayo ya kifahari ambayo yeye anayaita kuwa ni ya kawaida.
"Kwanza si magari ya kifahari, wewe ndiye unayeyaita hivyo, ni kwa sababu ya umasikini wetu tu, lakini lazima waziri atembelee gari lenye hadhi yake," alisisitiza Chenge.
Hata hivyo, aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo kabla ya Chenge, Basil Mramba aliwahi kukaririwa na gazeti hili kuwa mashangingi ni mzigo mkubwa kwa serikali na kwamba inafanya mipango ya kusitisha ununuzi wa magari hayo.
Alipoulizwa haoni huo umasikini wa nchi yetu ndiyo ambao ulitupasa kuacha kununua magari hayo, alijibu, " kwanza, matumizi ya serikali hayawezi kuzidi kwa ajili ya magari haya", na kuhoji:
"Hivi siku za nyuma katika serikali zilizopita mafuta yalikuwa yakitolewa lita 50 kwa wiki, nchi yetu ilipiga hatua gani kubwa katika nyanja za maendeleo?" Chenge alipoelezwa mfano, wa serikali ya Mwalimu Nyerere kwamba iliweza kujenga viwanda na mashirika makubwa ambavyo watawala wa sasa wanayauza ovyo, alijibu tena, " wewe sikia, haya mafuta ya magari hayawezi kukuza uchumi, cha msingi watu fanyeni kazi kwa bidii, tushirikiane kutekeleza ilani ya chama na mipango ya maendeleo ya serikali."
Hata hivyo, Chenge alisema serikali itachukua hatua kwa wale watakaobainika kutumia magari hayo katika mabaa na nyakati zisizo za kazi.
Wakati huo huo; Shirika la Fedha Duniani (IMF) limeishauri Serikali ya Tanzania kubana matumizi yake kwa kuyaelekeza fedha kwenye vipaumbele muhimu vya nchi kama afya, miundombinu, elimu na maji.
Ushauri huo ulitolewa jana na Mwakilishi Mkazi Mwandamizi wa IMF nchini, Dk David Robinson, alipokuwa akijitambulisha kwa wanahabari jijini Dar es Salaam, katika ofisi ya shirika hilo.
"Siwezi kulitolea maoni kwa undani kwani nahitaji muda wa kujifunza zaidi, lakini ni muhimu Serikali ikadhibiti matumizi yake ya fedha na kuzielekeza katika sekta muhimu kama afya, miundombinu, elimu na maji," alishauri Mwakilishi huyo wa IMF.
Dk Robinson alisema hayo wakati akijibu hoja ya wanahabari juu ya ripoti ya IMF kuhusu hali ya uchumi wa Tanzania, ambayo imeifagilia Serikali kuwa iko makini katika udhibiti wa fedha, wakati ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeonyesha kuwepo kwa mushkeli katika matumizi.
Ripoti hiyo ya CAG ya hivi karibuni inaonesha kwamba Serikali imekuwa na matumizi makubwa kwa kutumia ziada ya sh900 bilioni miezi minne kabla ya kuisha kwa mwaka wa fedha. Taarifa ya CAG kwa mwaka 2005/06, inaonesha kuongezeka kwa matumizi ya kawaida kutoka Sh2,138,860,343,786 mwaka 2004/05 hadi Sh2,732,455,841,323 mwaka 2005/06.
Taarifa hiyo inasema, fedha za matumizi ya miradi ya maendeleo zimepungua kutoka Sh850,533,139,955 mwaka 2004/05 hadi Sh844,103,204,420, huku deni la taifa la nje likikua hadi kutokaSh5,548,446,077 hadi Sh5,772,620,992 katika kipindi hicho na kumfanya Rais Jakaya Kikwete kuitisha mkutano na watendaji waandamizi wa serikali kuijadili katika kikao hicho kilichofanyika Dodoma, ambapo aliwatahadharisha watendaji watakaorudia makosa hayo watatimuliwa kazini.
Takwimu zilizotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Machi mwaka huu, zinaonesha tayari katika matumizi hayo kuna ongezeko la asilimia 5.6 ya pato la taifa, badala ya asilimia 5.1 ya pato la taifa kama ilivyokuwa imekadiriwa kwenye bajeti ya mwaka 2006/07.
Kutokana na kuongezeka kwa matumizi hayo, taarifa ya hiyo ya BoT inaonyesha mpaka Februari mwaka huu, tayari kumekuwa na pengo la Sh978.8 bilioni.
Akizungumza zaidi, Dk. Robinson alieleza kwamba kwa sasa jumuiya ya nchi wahisani imekuwa ikielekeza zaidi misaada yake ya fedha kwenye bajeti kuu za Serikali ili ziwe na uhuru wa kupanga vipaumbele vyake badala ya kuamuliwa.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika hilo ya Februari mwaka huu Bodi tendaji ya IMF imeridhia kuipa Tanzanai fedha zaidi baada ya kuridhishwa na inavyotekeleza Mkakati wake wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umasikini (MKUKUTA) katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita .
Kwa hali hiyo Tanzania imefunzu kupewa dola za kimarekani 4.2 milioni kwa ajili ya kuendeleza jitihada hizo. Kiasi hivyo kinafanya jumla ya fedha ambazo Serikali ya Tanzania itazipata kwa ajili ya mpango huo kufikia dola za kimarekani 29.4 milioni.
Lengo la wahisani hao ni kuona kwamba uchumi wa Tanzania unakuwa hasa katika kujenga uwezo wa matumizi bora ya fedha, kuimarisha mchango wa sekta ya fedha katika maendeleo, kuwa na sera za fedha zinazotekelezeka na mazingira bora ya biashara.
Ripoti hiyo imeonesha kwamba katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Uchumi wa Tanzania umekuwa ukikuwa vizuri na kufanikiwa kushusha mfumko wa bei pamoja na kujiwekea hakiba kubwa ya fedha.

Reply With Quote




Follow Us Here