TANZANIA UKABILA HAKUNA?
AU KUNA RUSHWA TU?
Duru za Kenya: Ukabila unavyotafuna siasa za nchi
Na Danny Mwakiteleko,Nairobi

MOTO wa uchaguzi unazidi kuchochewa nchini Kenya, hasa baada ya Rais Mwai Kibaki, hatimaye kuwatangazia Wakenya kuwa anataka apewe miaka mingine mitano ya kuiongoza nchi, katika kile anachosema ni kukamilisha mipango yake ya maendeleo aliyoianzisha.


Tayari habari za Kibaki kusimama kwa tiketi ya Muungano wa Vyama ujulikanao kama Party of National Unity (PNU) ikiwa na maana ya Chama cha Umoja wa Kitaifa, zilishaandikwa sana na vyombo vya habari, wiki kadhaa kabla Rais Kibaki (76), hajatangaza uamuzi wa kugombea urais kwa mara ya pili katika ukumbi wa Jengo la Ukumbi wa Mikutano la Kenyatta (KICC) Jumapili iliyopita.


Tayari sasa kila Mkenya amekuwa akizungumzia namna uchaguzi wa mwaka huu utakavyokuwa, huku kila mmoja akitabiri kwa vigezo vyake mwenyewe, ni mgombea yupi anaweza kuibuka mshindi na kuunda Serikali Januari mwakani.


Ukifuatilia ubishi mitaani na hata wakati mwingine mazungumzo na mijadala ya kisomi, utabaini kwamba kila mtu anajaribu kuuangalia uchaguzi wa Kenya na matokeo yake juu ya mgombea yupi ataibuka mshindi, kwa mtazamo wa kikabila.


Wakikuyu wote kutoka Nairobi na Mkoa wa Kati wanaamini kabisa kwamba mgombea atakayeibuka mshindi katika uchaguzi wa mwaka huu ni Rais Mwai Kibaki, ambaye ni mzaliwa wa Nyeri katika Mkoa wa Kati.


Ukiwauliza vigezo wanavyotumia ni kwamba Rais ameongoza miaka mitano iliyopita kwa amani na kuiletea maendeleo Kenya bila upendeleo.


Ukiwauliza Waluo kutoka Mkoa wa Nyanza nani ataibuka mshindi, wote watakujibu bila kutafuna maneno kwamba kipenzi chao Raila Odinga wa ODM, ndiye atakayeibuka mshindi na kuunda Serikali Januari mwakani.


Ukiwauliza sababu ni kwamba Raila anastahili kuwa Rais kwa sababu ni miongoni mwa watu waliopigana na udikteta wa Daniel arap Moi kwa nguvu zote, ikiwa ni pamoja na kuwekwa kizuizini kwa muda mrefu.


Ukiwauliza Wakamba, wao pia wanaelekeza matarajio yao kwa Kalonzo Musyoka, anayewania urais kupitia ODM-Kenya, kwamba ndiye atakayeibuka na vifijo katika kinyang'anyiro hicho ambacho vyombo vya habari vya Kenya vimekiita 'mashindano ya farasi watatu.'


Ni wazi katika hali kama hiyo kwamba Raila Odinga atapata kura nyingi zaidi kutoka Mkoa wa Nyanza, Musyoka kura nyingi kutoka miongoni mwa Wakamba wakati mtetezi wa kiti hicho, Mwai Kibaki, anatarajia kupata kura nyingi kutoka Mkoa wa Kati.


Pengine mmoja wa walijitoa mhanga katika siasa za kikabila za Kenya ni Uhuru Kenyatta, ambaye amelazimika kumuunga mkono Rais Kibaki kwa kuhofia kupoteza hata ubunge wake, iwapo angesimama kuwania urais kwa kuwa Wakikuyu wangemwona kama msaliti anayetaka kupunguza kura za Kibaki.


Wagombea wote watatu sasa wanapigania kugombea kura kutoka katika mikoa mingine, hasa wa Bonde la Ufa, mkoa mkubwa kuliko yote ambao takwimu za Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK) zinaonyesha kuwa ndio wenye wapigakura wengi kuliko mikoa mingine yote. Mkoa huo una wapigakura zaidi ya milioni tatu.


Ukitaka kujua namna siasa za kikabila zilivyojichimbia miongoni mwa Wakenya, basi jaribu kupitia hotuba za wagombea hao wakati wakiwashukuru wajumbe kwa kuwachagua kupeperusha bendera za vyama vyao katika uchaguzi wa baadaye mwaka huu, Raila na Kalonzo walikemea hisia hizo, wote wakiahidi kujenga Kenya inayojali utu wa mtu na si kabila lake.


Raila alikwenda mbali zaidi na kulaani maneno yanayozungumzwa mitaani kwamba mtu ambaye hajatahiriwa hawezi kuwa kiongozi wa nchi, akisema siasa za aina hiyo haziwezi kuifikisha mbali Kenya kwa kuwa ndizo zinazojenga chuki miongoni mwa watu wa makabila mbalimbali.


Hata Rais Kibaki wakati akitangaza kugombea urais kwa mara ya pili Jumapili iliyopita, naye alivifananisha vyama vingine kama makundi ya kikabila ambayo viongozi wake ni wapayukaji zaidi kuliko watendaji na kwamba watadhoofisha jitihada alizozifanya katika kipindi chake cha uongozi.


Hata hivyo, jambo ambalo Wakikuyu na Wakamba wanakubaliana ni kwamba ni afadhali Kibaki au Kalonzo wachaguliwe kuwa Rais. Wengi miongoni mwa makabila hayo mawili wanaamini kwamba iwapo Raila ataibuka mshindi, basi nchi itakoma kwa vituko vya watu wa kabila la Waluo.


Waluo ni kabila ambalo Wakenya wengi wanaamini kwamba ni wajivuni wa kupindukia na kwamba pamoja na wengi kupata nafasi ya kusoma ndani ya nje ya nchi, bado wanayo tabia ya kujiona wao ndiyo kabila bora kuliko makabila mengine ya Kenya.


Ndiyo maana basi Wakamba wanaweza kusamehe Kalonzo Musyoka akishindwa urais na baadhi yao wakampa kura Mwai Kibaki, lakini kamwe hawaamini kwamba Raila Odinga, hasa baada ya kufarakana na Kalonzo, anaweza kuwa Rais wa Kenya na nchi ikatawalika kwa amani.


Kwa kifupi hiyo ndiyo sura halisi ya siasa za Kenya, nchi ambayo kiuchumi imepiga hatua kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki, lakini ambayo kiongozi hachaguliwi kutokana na sifa zake pamoja na sera za chama chake, bali kutokana na mazingira ya kisiasa ya wakati huo pamoja na hisia za kikabila zinazotawala.


Pamoja na Watanzania kutamba katika ukanda huu wa Afrika kwa kudhoofisha nguvu siasa za kikabila, zipo dalili za wazi zinazoonyesha kuwa itafika wakati kiongozi atakuwa akichaguliwa si kutokana na uwezo, haiba au uzalendo wake, bali mahali anakotoka. Tuombe Mungu tusifikie huko kwani udhaifu wa siasa za aina hii sote tunautambua.


Kwa kifupi ni kwamba katika siasa za aina hii, ufisadi wa hali ya juu pamoja na upendeleo wa waziwazi katika nyanja zote za maisha hutawala na matokeo yake ni kuibuka kwa chuki baina ya watu wa kabila moja na jingine na hatimaye kusababisha kuzorota kwa usalama na ustawi wa maisha ya watu.

source: http://www.mwananchi.co.tz/newsre.asp?id=1868