WIKI kadhaa zilizopita nilialikwa katika mkutano wa vijana uliofanyika Arusha, ambako nilikwenda kama mzungumzaji.
Katika mazungumzo yetu, kijana mmoja aliuliza swali kuhusu sababu za Tanzania kuendelea kuwa taifa masikini.
Bila shaka hata wewe unayesoma makala haya, ni kati ya Watanzania ambao wamekuwa wakijiuliza; kwa nini Taifa hili bado ni duni? Achilia mbali Tanzania bara ambalo ni eneo kubwa, vipi kuhusu eneo dogo kama Zanzibar?
Unakuta eneo fulani lina utitiri wa viongozi kuanzia balozi wa nyumba kumi, Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa, Mtendaji wa Kata, Diwani, Mbunge, Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa, Mwenyekiti wa Halmashauri na viongozi wengine, lakini bado eneo linaendelea kuwa duni. Tatizo ni nini?
Hivi ni kwa nini maeneo mengi ya Zanzibar kasi ya wasio na ajira ni kubwa, wakati kisiwa hicho kikiwa na wakazi wachache? Ni swali ambalo kila mwenye akili timamu anaweza kujiuliza.
Hata Tanzania bara, bado tunaweza kuendelea kujiuliza kwa nini hali ya maisha ya walio wengi ni duni wakati tumekuwa tukiahidiwa mengi hasa nyakati za kampeni?
Nafikiri shida kubwa iliyoko Tanzania ni kushindwa kuthubutu; kuna Watanzania wengi ambao hawajiamini kuanzisha mambo.
Kwa mfano, wahitimu wengi wanafikiri kilicho muhimu kwao ni kuajiriwa. Mtu anaweza kusomea sheria, lakini yuko tayari kufanya kazi hata ya kuuza duka kwa sababu ndio kazi aliyopata ya kuajiriwa.
Wengi wanafikiri kuajiriwa ndio maisha lakini tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa watu ambao maisha yako yote wanategemea ajira, ndio ambao hufa wakiwa maskini.
Kwa nini? Nakubaliana na hili kwani ni ukweli kuwa baada ya kumaliza ajira, kinachofuatia ni kupewa posho zako na kurudi nyumbani. Hakuna njia nyingine ya kuweza kuishi zaidi ya kusubiri kifo, huku ukila mafao yako.
Hata kama wewe ni Mbunge, Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa, kazi hiyo bado haina chochote kama hutakuwa na kitu kingine cha kufanya.
Kuna watu ambao walikuwa wakuu wa wilaya, leo hii wanafanya biashara ya mama ntilie. Kuna watu walikuwa wana fedha, leo hii hata nauli ya daladala kwenda huku na kule ni shida.
Ndugu yangu ni lazima kuwa makini na kufikiria kuanzisha miradi yenye maana. Miradi mizuri zaidi, miradi ambayo inaweza kweli kusaidia kukufanya kuwa na mafanikio zaidi.
Ni vigumu kufikiri kwamba unaweza kuwa na maendeleo makubwa, ikiwa fikra zako za aina ya miradi ni kuhusu miradi yenye kukuletea mafanikio madogo.
Ni kwamba unaweza kuanza kwa miradi yenye fedha ndogo, nikimaanisha kwamba anzisha mradi kulingana na fedha ulizonazo, lakini lililo la msingi ni kuangalia aina ya miradi ambayo inaweza kuleta mafanikio makubwa zaidi mbele.
Ninachotaka kueleza hapa ni kwamba sababu kubwa ya Tanzania kuendelea kuwa maskini ni wananchi wenyewe kutokuwa na uelewa wa nini ambacho wanatakiwa kufanya ili kuwa na maendeleo. Katika hili inawezekana hata walio madarakani nao hawakuwa na uelewa juu ya hilo.
Hata baada ya baadhi ya viongozi kuanza kufahamu umuhimu wa namna ya kuwafanya wananchi kuwa na maendeleo ya haraka, wengi walishindwa kufanya mikakati hiyo kwa staili inayotakiwa.
Uongozi usiofaa au viongozi wasiofaa, kwa maana ya kuwa na watu ambao wanashindwa kuwaendeleza wengi, ni kati ya sababu za msingi za kudumaa kwetu kimaendeleo.
Kwa nini tumsifie mwalimu kuwa anajua kufundisha ikiwa idadi kubwa ya wanafunzi wake wanafeli mitihani?
Hata kama labda mtoto mwenyewe anayefundishwa, kichwani anasumbuliwa na kero nyingi na kusababisha ashindwe kusoma vizuri, bado hatuwezi kusahau mchango wa mwalimu kwa kufeli mwanafunzi huyo.
Ndiyo maana nasema kwamba umasikini unaoendelea Tanzania unachangiwa na viongozi wasio na huruma na wananchi. Hawana mikakati mahsusi katika kusaidia maendeleo katika maeneo wanayoyaongoza.
Aidha, Watanzania wengi bado ni wazito katika kupambanua mambo. Msingi hasa wa kuwa na maendeleo ni pamoja na kutokuwa na urafiki wa kudumu au uadui wa kudumu na wanasiasa.Mataifa mengi yaliyoendelea tabia zao ni kwamba hawana urafiki wa kudumu wala uadui wa kudumu.
Kwa mfano, kinachoendelea Zanzibar sio sahihi hata kidogo, kwamba kila uchaguzi, ni lazima kuona Pemba inachukuliwa na CUF, Unguja inachukuliwa zaidi na CCM. Au hata kwa Tanzania bara, ni makosa mno kukubali kuendelea kukipigia kura chama fulani miaka nenda miaka rudi.
kwa mfano, kama katika uchaguzi uliopita ulikipigia kura Chadema, TLP au CCM, ni muhimu katika uchaguzi ujao, kumpima kiongozi alifanya nini kabla ya kupiga kura yako.
Kama hajafanya chochote, hakuna sababu ya kukipigia kura wala kumpigia kura mgombea wake ambaye ameshindwa kutekeleza ahadi alizotoa katika uchaguzi uliopita.
Chanzo: hapa

Reply With Quote


Follow Us Here