Lipulipu usilale, CCM bado tele,
Vijijini wengi tele, fanya hima twende kule,
Nikote si peke Hale, mambo bwana Lipu kule,
CCM namba wani, vijijini masikani.
Usiamini mayowe, ukahisi mwambawewe,
Kura Bwana si mayowe, kura ni tiki upewe,
CUF bado utambuwe, kina mama wambiwe,
CCM namba wani, vijijini masikani.
Kura ziko vijijini, kura haziko mijini,
Mijini bwana rahani, kupiga hawatamani,
Mijini ushabikini, si watu wakuamini,
CCM namba wani, vijijini masikani.
Utangaze matawini, wote wawe safarini,
Wote kwenda vijijini, wakafanye kampeni,
Sivyo Lipu hutawini, amini hiloamini,
CCM namba wani, vijijini masikani.
Nenda nawe vijijini, watuwawe na imani,
Wakujue waamini, wajue wasema nini,
Sivyo baba naamini, hutashinda abadani,
CCM namba wani, vijijini masikani.
CCM namba wani,huko kote mashambani,
Wapinzani ndio nini, watavuruga amani!,
Kwanza CUF cha udini, wanasema vijijini!,
CCM namba wani, vijijini masikani.
Wamechoka naamini, watu wote vijijini,
Tatizo kukuamini, ukifuzu tutawini,
Lipumba baba amini, mambo iko vijijini,
CCM namba wani, vijijinimasikani.
Tangaza wajemjini, watu wako vijijini,
Sema bendera shikeni, rudi sasa vijijini,
Matawi kafungueni, HAKI SAWA tangazeni,
CCM namba wani, vijijini masikani.
Baba niko ukingoni, Lipu yangu yashikeni,
CUF mimi idamuni, ikishindwa nitabuni,
Kwani mwingine sioni, na hofu uchumi duni,
CCM namba wani, vijijini masikani.
Beti kumi kaditama, zanitosha mie mwana,
Fatuma Magimbi mama, msalimu sanasana,
Azidi mama kusema, Bunge azidilibana,
CCM namba wani, vijijini masikani.

Reply With Quote
Follow Us Here