na Mwandishi wetu, Shinyanga
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja ameituhumu kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick kwa kuchimba madini ya fedha na shaba kinyemela.Mgeja ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Taifa, amedai kuwa kampuni hiyo pia imekiuka mkataba wake, na sasa inachimba dhahabu nje ya maeneo iliyopewa rasmi.Mwenyekiti huyo ametoa tuhuma hizo juzi katika kikao cha ushauri cha mkoa, akisema zipo taarifa za uhakika kuwa mwekezaji ameingia katika eneo kubwa mno, nje ya lile alilopewa kisheria, na kwamba amekuwa akichimba chini kwa chini umbali mrefu.“Kuna taarifa za vijana wetu zinaonesha kuwa Barrick sasa amekwenda umbali mrefu sana wa zaidi ya kilometa nne na karibu ataingia Mkoa wa Geita.“Hakuna ubishi kwamba huu ni wizi, lazima ufanyike uchunguzi wa haraka, tukiacha wizi huu uendelee, ipo hatari ya vizazi vijavyo vikatusuta,” alisema Mgeja.Alikiri kuwa maisha ya Watanzania wanaoishi jirani na maeneo ya migodi ni magumu kiuchumi, wakati mwekezaji anajipatia kipato kikubwa kutoka katika madini ya shaba na fedha ambayo halipii chochote serikalini.Aliishauri serikali kupitia upya mkataba wa mwekezaji huyo wa Bulyanhulu ili aweze kulipa mrabaha mwingine kutokana na madini ya shaba na fedha anayoyapata kutoka katika mgodi huo wa dhahabu anaoumiliki hivi sasa.Taarifa hiyo iliwashitua baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo ya ushauri ya mkoa, na kutaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya mwekezaji huyo.


Reply With Quote


Follow Us Here