Na Nizar Visram

KUNA kampuni za kimataifa ambazo huwa zinatumia madeni ya nchi za ulimwengu wa tatu kama njia ya kuzikamua nchi hizo.

Mojawapo ni Donegal International, inayomilikiwa na raia wa Marekani aitwaye Michael Sheehan. Kampuni kama hizi huitwa “mfuko wa tai” (vulture fund) au labda tungewaita mafisi wanaosubiri nchi zinaelemewa na madeni ndipo wanapozitia kabari.

Hivi ndivyo ilivyofanyika kwa Zambia. Katika Mahakama Kuu jijini London kampuni hiyo ya Donegal imeishitaki Zambia kwa deni la dola 40 milioni pamoja na riba.

Mwaka 1979 serikali ya Romania iliikopesha Zambia matrakta. Zambia ilishindwa kumaliza kulipa deni na mnamo 1999 nchi hizo mbili zilikubaliana kuwa Zambia ilipe dola milioni tatu na wamalizane.

Lakini kabla ya kumalizana Donegal ikaingilia kati. Ikanunua deni la Zambia kutoka Rumania iliyokuwa ikiidai Zambia. Deni lenyewe ni la dola 30 milioni. Donegal ilinunua deni hilo kwa dola milioni tatu na kisha ikafungua kesi mahakamani na kudai deni lote lilipwe pamoja na riba na gharama ya kesi. Jumla ya malipo ikafikia dola milioni 55.

Malipo yote hayo yanayodaiwa ni zaidi ya deni la Zambia lililoahidiwa kufutwa kwa mujibu wa ahadi iliyotolewa na nchi tajiri (G8) huko Gleneagles mnamo mwaka 2005. Yaani nchi tajiri sasa zitakuwa zinachukua zaidi ya kile wanachosamehe.

Katika kesi hiyo ya madai Zambia inawakilishwa na wakili wake William Blair QC ambaye ni ndugu yake Waziri Mkuu Tony Blair.

Hukumu ikiwa inasubiriwa Jaji ameagiza kuwa mali zote zinazomilikiwa na Zambia huko Uingereza zidhibitiwe mpaka hapo uamuzi utakapotolewa.

Katika idhaa ya BBC iliripotiwa kuwa barua iliandikwa na Sheehan kwenda kwa aliyekuwa Rais wa Zambia wakati huo Frederick Chiluba akimpa ‘ofa’ ya dola milioni mbili wakati Donegal iliponunua deni la Zambia. Wakili Blair alisema hiyo ni rushwa aliyopewa Rais wa Zambia, lakini BBC ilipomuuliza Sheehan alieleza kuwa eti ni fedha za ‘sadaka’ alizopewa Chiluba azifikishe kwa wahusika.

Kwa mujibu wa sheria ya Marekani rushwa inayotolewa na kampuni ya huko kwa mtu yeyote nje ya nchi ni kosa la jinai. Hii ni chini ya sheria iiitwayo ‘Foreign Corrupt Practices Act’ Haieleweki iwapo Donegal na Sheehan watashitakiwa huko Marekani.

Mbinu hizi chafu zimelaaniwa na mashirika na wanaharakati wengi duniani. Wamezitaka nchi ‘tajiri’ kuzuia mtindo huu hasa kwa vile nchi hizo zimekuwa zikidai kuwa zinafuta madeni ya nchi wanazoziita ‘masikini.’

Shirika la misaada la Oxfam limesema kuwa Donegal inaikaba Zambia wakati nchi hiyo inasemekana imefutiwa madeni yake na nchi tajiri. Sasa ni nchi hizo hizo zinaruhusu mafisi wa kimataifa kuzikaba nchi kama Zambia.

Naye Waziri wa Fedha wa Uingereza, Gordon Brown alikubali kuwa kampuni hizi za kifisi zina malengo ya kuzifilisi nchi maskini kwa kuwapokonya fedha ambazo zingetumika katika ujenzi wa shule na hospitali. “Ni jambo lisilokubalika kimaadili,” anasema Brown.

Anasema mifuko hii ya tai ni makampuni yanayonunua madeni ya nchi masikini kwa bei rahisi hasa wakati madeni hayo yanapokuwa yanafutwa au kusamehewa. Baada ya kuyanunua huenda mahakamani na kudai walipwe deni lote pamoja na riba. Matokeo yake ni kuwa nchi mdaiwa hulipa mara kumi zaidi ya mkopo uliokopwa.

Kesi hii kuhusu deni la Zambia ni moja tu kati ya mengi mengine. Huko New York kuna bepari mkubwa bilionea ambaye ndiye aliyeanzisha ‘biashara’ hii ya mfuko wa tai. Mwaka 1996 kampuni yake ilinunua deni la Peru kwa dola milioni 11 na kisha ikaishitaki nchi hiyo ilipe deni zima la dola milioni 58 au nchi ingefilisiwa. Peru ikalazimishwa kulipa fedha hizo.

Sasa kampuni hiyo inaishitaki Congo Brazzaville. Ilinunua deni lake la dola milioni 400 kwa bei ya dola milioni 10. Nchi hiyo sasa inashitakiwa ilipe deni lote pamoja na riba.

Kwanini basi makampuni haya ya kifisi hayazuiwi au kukemewa na Serikali yao ya Marekani? Ni kwa sababu kuna mbinu inayotumika.

Makampuni haya yana umoja wao unaoitwa shirika la washauri wa madeni ( Debt Advisory International) nalo humwaga fedha kemkem. Wamekuwa wakilipa dola 240,000 kila mwaka kwa kampuni ya ushawishi (lobbyists) jijini Washington iitwayo Greenberg Traurig. Hivi karibuni ofisa mkuu wa kampuni hiyo alikamatwa.

Mshawishaji mwingine ni Paul Singer ambaye ana mahusiano ya karibu na wanasiasa wa Republican. Amekuwa mfadhili mkubwa kuliko wote aliyetoa dola milioni 1.7 tangu Rais George Bush aanze kufanya kampeni ya urais.

Paul Singer pia ameahidi kutoa dola 1.5 milioni kwa kampeni ya Rudi Guiliani ambaye inasemekana huenda akawa mgombea urais kwa niaba ya chama cha Republican.

Makampuni haya yameajiri mawakili ambao kazi yao ni kuchunguza madeni ya nchi masikini na kuona kama madeni yenyewe yanaweza yakanunuliwa na kisha mali zao zilizo nchi za nje zikamatwe na kufilisiwa kwa amri ya mahakama

Mbinu hizi hazitumiwi tu na makampuni haya ya tai. Hata serikali za nchi tajiri pamoja na mabenki na makampuni yao ya kibiashara hutumia mbinu kama hizo.

Mwaka 2003, kwa mfano, Benki ya Dunia (WB), Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Serikali za nchi tajiri ziliidai Ethiopia dola 73 milioni pamoja na riba wakati nchi hiyo ilikuwa imekumbwa na njaa. Hii ilifanyika wakati nchi tajiri zilikubaliana kusamehe madeni ya nchi masikini zisizokuwa na uwezo wa kulipa.

Nchi saba tajiri (G7) ziliahidi kufuta madeni ya dola 100 bilioni. Chini ya mpango huu uliofikiwa Cologne mwaka 1999, nchi 26 ziliahidiwa kufutiwa madeni ya dola 68 bilioni. Lakini kufikia 2003 ni nusu tu ya madeni hayo yalifutwa.

Kwa upande wa Ethiopia ahadi zote hizo za G7 hazikusaidia na mwishowe nchi hiyo ikalazimishwa kulipa dola 100 milioni wakati wananchi wake walikuwa wameandamwa na njaa isiyopata kuonekana katika muda wa miaka 20.

Ethiopia haikuwa nchi pekee, nchi zingine tatu za Kiafrika zilizokuwa zikikabiliwa na njaa, Zambia, Msumbiji na Malawi, nazo zilikabwa na kulazimishwa kulipa dola 250 milioni kwa wadai wakati walipokuwa wanaomba msaada wa chakula.

Halafu wakati huo huo wanapofuta hayo madeni wanazikamua nchi za ulimwengu wa tatu kwa kutumia mbinu za biashara. Kwa mfano Uganda ni nchi ya kwanza kupita ‘mtihani’ wa G7 unaoitwa HIPC na wakaisifu sana. Ikaahidiwa msamaha wa dola bilioni moja, lakini wakajikuta bei ya kahawa yao imeanguka katika soko la kimataifa. Hivyo licha ya kufutiwa madeni ikaelemewa tena na madeni mengi zaidi.

Ethiopia nayo ilifutiwa madeni ya dola 30 milioni baada ya kupita vikwazo vya HIPC. Lakini ilikuwa ikilipa maradufu katika matumizi yake ya matibabu tu. Asilimia 5 ya kodi iliyokusanywa ilitumika kulipa madeni ya kimataifa. Nusu ya watoto wake walikuwa na utapiamlo na zaidi ya asilimia kumi walifariki kabla ya kufikia umri wa miaka mitano. Ilihitaji dola 73 milioni kulipia chakula kwa wananchi wake milioni 12.

Kwa hiyo kufutiwa madeni kulikuwa ni danganya toto tu kama ilivyo kwa mataifa mengine ya Kiafrika.

Kuna mbinu nyingine inayofanya ufutaji wa madeni kuwa ni udanganyifu mkubwa kwa nchi masikini. Hii ni njia ya rushwa zinazotolewa na nchi tajiri kwa watawala wa nchi masikini. Kwa njia hii nchi masikini zinazidi kujikuta zina madeni. Wakati wa kuuziwa rada au ndege ya Rais au helikopta za kijeshi, njia zote hizo hutumika kuzipora nchi masikini. Hapa tunazungumzia uporaji wa mabilioni ya dola kwa njia ya kile wanachoita kamisheni ambayo kwa lugha sahihi ni rushwa.

Vyama vya kiraia (NGO) katika nchi za G7 vimetoa ripoti inayosema kuwa iwapo G7 zinasema kweli kuhusu kupiga vita rushwa na ufisadi, basi ni vizuri zianzie na madeni yake yote tangu miaka ya nyuma na kufanya utafiti ili kujua chimbuko la madeni yote. Ripoti hiyo inazungumzia madeni haramu yanayodaiwa na nchi kama Canada, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Italia, Japani na Marekani.

Haya ni madeni ambayo yalitokana na mikopo kwa watawala wala rushwa na waporaji. Wakopeshaji walijua haya na hata waliwahimiza watawala waingie katika madeni haya haramu, wakijua fika kuwa wananchi hawangenufaika hata kidogo na kuwa fedha hizo zingeishia katika akaunti zao huko Uswisi, Paris au London. Lengo lilikuwa ni kuyasaidia makampuni ya Ulaya kufanya biashara kwa njia za kijanja.

Gail Hurley, afisa wa sera wa NGO iitwayo Eurodad anasema: “Wakopeshaji wanapaswa wawajibishwe kwa uamuzi mbovu wa kutoa mikopo mibovu. Wanasiasa wa Ulaya wamecharuka na suala la rushwa na utawala bora katika nchi masikini. Ni sawa, lakini Serikali zetu zitakuwa zinatudanganya iwapo hazitaanzia kwenye chanzo cha deni. Haikubaliki hata kidogo kwa Serikali za G7 kuhubiri utawala bora wakati zinakusanya madeni yaliyotokana na uamuzi wao mbovu.”

Kwa mfano, Ujerumani iliiuzia Indonesia iliyokuwa ikitawaliwa na dikteta Jenerali Suharto manowari ya kijeshi wakati nchi hiyo haikuwa ikikabiliwa na adui yeyote wa kigeni, ila tu ilikabiliwa na upinzani mkali katika jimbo la Timor Mashariki iliyokuwa imeivamia kijeshi. Silaha alizopewa dikteta Suharto kutoka mataifa ya G7 alizitumia kukandamiza wananchi wa Indonesia na Timor.

Halafu Suharto pia alikopeshwa na Japani mradi wa madini ya alumini (aluminium), siyo kwa manufaa ya Indonesia bali kwa faida ya wasafirishaji wa madini hayo huko Japani.

Serikali ya Ufaransa nayo iliunga mkono mabenki yake yalipoifilisi Congo-Brazzaville. Serikali hiyo kwa kupitia shirika lake la misaada ilitoa mkopo kwa Congo(B) na baadaye kampuni ya ElfCongo iliingia kati na kufilisi mafuta ya nchi hiyo.

Serikali ya Uingereza ilidhamini mkopo wa benki ya kibiashara kwa Kenya ili kutumia kulipa kampuni ya Kiingereza iliyotoa ‘ushauri’ kwa Kenya. Malipo hayo yalizidishwa kwa zaidi ya mara tano ya kima ambacho kingelipwa kwa kawaida.

Canada ikadhamini ujenzi wa bwawa la Yacyreta huko Argentina na Paraguay wakati ilieleweka wazi kuwa watawala waliokuwa madikteta wa kijeshi walikuwa wanapora mabilioni ya dola kutoka mikopo ya kigeni.

Ripoti ya NGO inataka madeni kama haya yote yachunguzwe na wakaguzi wasiofungamana, ili kuona ni kiasi gani cha mikopo ilitolewa na Serikali na mabenki kwa njia za hadaa na udanganyifu. Wakati huo huo Serikali za G7 zinatakiwa zifuate mfano wa Norway ambayo hivi karibuni ilikubali kuwa nayo inawajibika kwa kutoa mikopo isiyolipika kwa nchi masikini.

Norway ilifuta madeni yake kwa nchi masikini.
Haya yalisemwa hivi karibuni na wanaharakati waliokuwa wakihudhuria mkutano wa kijamii wa kimataifa (WSF) uliofanyika jijini Nairobi.

Walitaka madeni yote ya kigeni yafutwe bila ya kuchelewa kwa vile madeni hayo ni haramu.
Aliyeongoza katika mwito huo ni Wangari Maathai ambaye ni mwanamama jasiri mwanamazingira wa Kenya anayesifika kimataifa. Aliuambia mkutano wa WSF: “Si jambo la siri kuwa mikopo mingi ilitolewa kwa watawala wa kidikteta wasiowajibika kwa wananchi katika Afrika na kwengineko. Na fedha hizo hazikuwanufaisha wananchi walengwa.”

Akaongeza “Unawezaje kuwabebesha mzigo wananchi masikini, mzigo wa kulipa mikopo ambayo ilitumika kuwagandamiza na kuwanyonya, iliyotumika kuwatajirisha watu wachache badala ya kuitumia kwa maendeleo ya wananchi masikini? Mikopo hii ni haramu”

Hotuba yake ilishagiliwa na maelfu ya washiriki wa mkutano huo. Ni vizuri ikumbukwe kuwa wakati wanaharakati akina Maathai walipokuwa wakikutana katika WSF huko Nairobi na watawala nao walikuwa wakikutana katika mkutano wao wa kiuchumi au WEF huko Davos.

Jambo linalosikitisha ni kuwa mzigo huu wa madeni unazidi kuongezeka na kuwaelemea wananchi masikini. Mkutano wa Nairobi uliambiwa na Joel Virado ambaye ni mjumbe wa Baraza la Wawakilishi nchini Phillipines kuwa deni la nchi yake limeongezeka kutoka dola 599 milioni mwaka 1965 hadi kufikia dola 60.1 bilioni hivi sasa.

Katika nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara nako mzigo wa madeni unazidi kuongezeka na sasa umefikia takribani dola 210 bilioni. Hii ni asilimia 85 ya uzalishaji wa mwaka mzima. Asilimia 64 ya walioathirika na Ukimwi duniani wanaishi katika nchi hizi. Kushindwa kulipa madeni maana yake ni kuwa waathirika hawa wanashindwa kupata madawa ya kurefusha maisha (ARV) kwa sababu bei zake zinazidi kuongezeka katika soko la kimataifa.

Sera za nchi hizi zimefungamana na madeni, kwani wakopeshaji wanalazimisha Serikali zifuate ushauri wao kama vile ubinafsishaji wa huduma za matibabu na soko huria. Si ajabu wananchi wa kawaida wanashindwa kupata matibabu kwa sababu wanashindwa kulipia madawa yanayouzwa kwa bei ya juu na makampuni ya kimataifa.

Kwa jinsi hali ya mambo ilivyo hivi sasa inakisiwa kuwa nchi zaidi ya 60 za Kiafrika zitashindwa kutimiza malengo la milenia ifikapo 2015. Nchi za G8 (Marekani, Urusi, Ujerumani, Ufaransa, Japani, Uingereza, Italia na Canada) ziliahidi kufuta madeni ya nchi 18. Kati ya hizo 14 ni za Kiafrika.
Lakini hii inafanyika kwa masharti ambayo kimsingi hayazinufaishi nchi wadaiwa. Maana yake ni kuwa nchi hizi zitaendelea kubaki masikini na zikidaiwa dumu daima.

Ni lazima madeni yote yafutwe, tukianzia yale madeni haramu ambayo hayapaswi kulipwa kamwe!

Wakati huo huo wananchi wenyewe wanapaswa waseme kwa sauti wasikike duniani. Wanapaswa kuziwajibisha Serikali zao kwa kuwabebesha madeni haramu.

Hatua moja iliyochukuliwa huko Kenya ni kuundwa kwa mtandao wa ufutwaji wa madeni (Kenya Debt Relief Network (KENDREN). Kazi yake ni kuchunguza na kukagua nyaraka za mikopo yote na kisha kuangalia mikopo hiyo ilitumikaje.

Mtandao huo unaelimisha wananchi na kushinikiza wabunge wapitishe sheria itakayozuia ulipaji wa madeni haramu, pamoja na uwazi katika mikataba ya mikopo.

Kenya hivi sasa inadaiwa dola 10 bilioni. Riba tu inachukua asilimia 22 ya bajeti. Fedha hizi zinaidhinishwa na Bunge. Hivyo Bunge lina haki ya kupata na kujadili mikataba ya mikopo bila ya visingizio vinavyotolewa na mawaziri.

Ulipaji wa mikopo unaidhinishwa na bunge lakini mikopo yenyewe ni siri ya mawaziri na vigogo wenzao.

Je hayo yanatuingia akilini? Kwa nini nasi tusiwe na vuguvugu kama hili la wenzetu?

[email protected]