|
Mapinduzi Bila Damu Wala Wafadhili

11th January 2007, 09:21 AM
Vunjavunja kila kitu. Madirisha ya vioo, pasua! Kama ni ya mbao, zing’oe kisha washia moto. Vunja kuta. Bomoa mageti. Ng’oa paa. Milango, tupilia mbali! Chomoa misumari yote. Badili kila kitu. Usiache chochote. Anza upya. Tunahitaji sera mpya, dira mpya, imani mpya, falsafa mpya, viongozi wapya, siasa mpya, fikra mpya. Hoji. Dadisi. Uliza maswali. Hoji kila mtu. Kila kitu. Hoji dini, siasa, sheria, imani, n.k. Jihoji wewe mwenyewe. Hatuwezi kuendelea kama tulivyo. Lazima tuanze upya.
Kwanini tunahitaji mwanzo mpya? Nitajibu swali hili kwa kutazama mifano michache. Tutazame vyombo vyetu vya habari. Kuna baadhi yetu ambao wanaamini kuwa vyombo vya habari Tanzania siku hizi vimepiga hatua mbele kimaendeleo. Hivi tunawezaje kujua kama vyombo vya habari vinapiga hatua mbele kimaendeleo? Tutafahamu kuwa vyombo vy ahabari vimeendelea kwa kutazama idadi ya magazeti, redio, vituo vya luninga, webu, n.k.? Je tutazame jinsi vyombo hivyo vinavyotupasha habari au tutazame habari vinavyotupasha? Kwa ujumla, maendeleo ya vyombo vya habari yanapimwa kwa vigezo vingi sana. Kigezo kimojawapo ambacho ni muhimu kwa gumzo la leo ni umuhimu wa habari/taarifa zinazotolewa na vyombo hivyo katika maisha ya binadamu.
Tazama habari yoyote kwenye gazeti kisha jiulize, je bila habari hii Watanzania tutashindwa kupambana na rushwa? Je habari hii inasaidia harakati za binadamu kuendeleza mazingira yake? Je habari hii inajenga utu wetu? Je bila habari hii taifa litakosa maarifa? Je habari hii akiisoma mwanangu itamsaidia katika ukuaji wa fikra zake na maendeleo yake shuleni? Je habari hii naweza kuichukua na kuibandika kanisani au msikitini ili waumini wenzangu waisome na kufaidika?
Ingawa Watanzania wengi tunajiita waislamu au wakristo, habari tunazopenda kusoma ni zile zinazohusu watu wanaovunja amri za mungu tunayemwabudu kuliko habari za watu wanaotii amri za huyo mungu wetu. Habari ya aliyefumaniwa na habari ya msamaria mwema ni ipi inapendwa zaidi? Nipe jibu la kweli.
Wenye magazeti yanayoitwa ya udaku wana hoja moja ambayo siyo ya kudharau. Wanawaambia wanaoponda magazeti yao kuwa wananchi wanapenda magazeti yao. Habari wanazoandika zinapendwa na Watanzania ndio maana magazeti yao yanazidi kushamiri. Wanachosema ni kweli. Hivi waumini wa dini mbili “kuu duniani” wakienda kununua gazeti, kukawa na gazeti moja linasema, “Dawa ya Ukimwi ni Kurani na Biblia,” na jingine linasema, “Kondomu Yapasuka: Mwanamke Aanguka Kilio.” Unadhani watanunua gazeti jipi? Je kama kuna gazeti lenye habari za mjadala wa wabunge kuhusu muswada wa marekebisho ya katiba na gazeti jingine lina habari ya mbunge aliyekuwa amelala wakati wa mjadala huo, unadhani Watanzania wengi watanunua lipi kati ya hayo mawili?
Ndio maana nasema inatupasa kuanza upya. Ni mara ngapi unatumia muda wako kusoma habari ambazo hazikufanyi uwe Mtanzania bora zaidi? Mara ngapi unatumia fedha zako kununua gazeti ambalo haliongezi maarifa na utu ulionao? Nenda kwa wauza magazeti katazame vichwa vya habari uone nafasi ya habari hizo katika juhudi zetu za kuondoa umasikini, uvivu, uzembe, rushwa, n.k. Sio ajabu kuwa asilimia 99 ya habari katika vyombo vya habari hazina nafasi yoyote katika harakati zetu za kuondoa umasikini. Ni habari ambazo hata tusipozijua hatutapoteza chochote. Tunapozijua tunapoteza kitu fulani: tunajaza akili zetu habari zisizo na nafasi katika sayansi ya maendeleo ya jamii na tunajaza nafsi na roho zetu habari zisizomtukuza yule tunayejifanya kumwabudu. Tunahitaji mapinduzi. Mapinduzi ya fikra. Mapinduzi ya namna tunavyoendesha maisha yetu.
Kuna watu wameshakata tamaa ya mapinduzi ninayozungumzia kwakuwa wanaona kila mtu amepotea, kila mtu anajali maisha yake binafsi, kila mtu anajali tamaa za mwili, n.k. Watu kama hawa wanadhani mabadiliko ya jamii yanahitaji kila mtu abadilike. Mabadiliko makubwa ya jamii huletwa na watu wachache sana ambao wanakuwa kama vile gonjwa la kuambukiza.Wanaanza kisha kila mtu anafuata.
Halafu kuna wengine wakisikia neno mapinduzi wanaanza kuhisi kuwa kinachozungumziwa ni umwagaji damu. Walioko madarakani wanaweza wakukamate kwa kutumia neno hili katika harakati. Sijui kwanini neno hili linatisha namna hii. CCM pekee ndio inaonekana kuwa ina haki ya kutumia hili neno. Wengine wakisikia neno mapinduzi wanaanza kuuliza fedha za kuleta hayo mapinduzi zitatoka wapi. Wanaanza kufikiria wazungu tunaowaita wahisani. Kumbe mwanzo mpya niaouzungumzia, mapinduzi ninayotangaza hayahitaji kumwaga damu, pesa za wafadhili, au nguvu za dola.
Mapinduzi haya hayataki makubwa. Yanahitaji uache kusoma habari zisizojenga fikra zako au utu wako. Tumia muda wako kujielimisha. Kurani inakwambia nenda hata China kutafuta hayo maarifa. Ukipata maarifa, waelimishe waliokuzunguka. Kama ni mzazi, gawa elimu hiyo kwa watoto wako mnapokaa mezani kula. Kama una watoto wadogo, wasomee vitabu vya maarifa usiku kabla hawajalala. Mapinduzi ninayoyazungumzia yamejengwa katika falsafa isemayo kuwa ukitaka kujua kilichoko ndani ya nafsi na akili ya mwanadamu, tazama mazingira yake. Kwahiyo kama unataka kubadili mazingira yake unaanza kwanza kubadili akili na nafsi yake. Jikwamue kiakili. Jikwamua kiroho.
Wanaharakati wengi ninaoshauriana nao kuhusu mwanzo huu mpya wanalalamika kuwa hawana uwezo, kwa mfano, wa kuwa na vyombo vya habari. Wanataka wapate chombo cha kuwasiliana na taifa zima. Wanataka taifa libadilishwe kwa wakati mmoja. Mtazamo huu tuuache. Huwa ninawauliza mifano ya vyombo wanavyozungumzia, wananitajia magazeti, redio, luninga, webu, n.k. Nawauliza, “Kuna chombo cha habari kikubwa kuliko mdomo? Kwa siku unasoma maneno mangapi na mangapi unasikia toka kinywani mwa watu?” Nawaambia kuwa midomo yao na midomo ya wengine kama wao ndio vyombo vya habari. Tayari wana vyombo vya habari ila hawajui. Kama huna uwezo wa kuanzisha gazeti au redio, tumia mdomo wako. Unaona kitabu kama kurani, kabla hakijaandikwa kilikuwa ni kumbukumbu katika akili za wafuasi wa mtume Muhammad. Walikuwa wakighani aya zake kama mashairi. Mdomo usiudharau.
Wengine wananiandikia wakiuliza, “Unajua braza mimi nina mawazo mengi napenda wananchi na vijana wenzangu wayajue lakini sina upenyo wa kuyatoa. Unaweza kunisaidia nipate safu kwenye gazeti kama wewe?” Nawauliza kama wamewahi kuandika hayo mawazo yao yakasomwa na marafiki zao wa karibu, majirani, vijana wenzie kijiweni, wanafunzi wenzao, waumini wenzao, ndugu zao na hata wazazi wao. Wananiambia kuwa mawazo yao hayajasomwa na watu hao maana hawajawahi kutoka gazetini. Nawauliza, “Hivi masomo shuleni unaandika wapi?” Wanajibu, “Kwenye daftari.”
Hapo tunakuwa tumefika kwenye kilele cha mazungumzo yetu. Kama mtu anaweza kuandika mambo kwenye daftari na yakasomeka, kwanini asitafute daftari zuri akaandika hayo anayotaka kuandika magazetini ili waliomzunguka waelimike? Kwanini asubiri hadi apewe safu gazetini? Asipopewa safu mawazo yake ndio yanapotea? Je kila mwelimishaji lazima awe na safu ili mawazo yake yawe na faida kwa binadamu? Kwanini unataka kukimbilia kuelimisha vijana nchi nzima wakati hujaelimisha hata vijana wenzako wanne mtaani? Kwani kuna ubaya gani ukiwa na daftari ambalo unaandika jambo jipya kila wiki? Hivi mambo ninayoandika katika safu hii ningeandika kwa mkono kwenye daftari yangepoteza maana yake?
Kijana, anzisha safu mtaani kwako. Usisubiri upewe safu gazetini. Kanunue daftari dukani. Andika, wape watu wasome. Usisumbuke na gazeti kwanza. Watu wa magazeti watakufuata. Kama kweli unataka kuleta mabadiliko anza na mtaa wako, usifikirie taifa. Mabadiliko ya nchi unayotaka hayatokei ghafla. Mabadiliko yanayoanzia mtaani ndio yanayobadili taifa. Ni kitu gani kinakuzuia kufanya mtaani kwenu unayotaka kufanya kwa Watanzania wote?
Taifa letu lina mtazamo wa ajabu kabisa wa maendeleo na demokrasia. Tunadhani maendeleo ni kama maembe mabivu. Maembe mabivu yako juu ya mti, ili tuyafaidi lazima yaje chini (yaanguke au tuyaangushe). Maendeleo kwetu yanatoka juu kwa viongozi na wasomi walioko juu. Maendeleo kwetu yanatoka juu kuja chini. Yanaanzia Dasalama kisha yanasambaa hadi mikoani. Huu sio mtazamo sahihi.
Tuna demokrasia ya kushushwa kama aya za manabii. Demokrasia ya kweli inaanza chini inakwenda juu. Demokrasia ya kweli ni pale mimi na wewe tunapoweza kufanya mwenyekiti wa mtaa atimize wajibu wake. Na aogope nguvu ya wana mtaa maana anajua kuwa asipotimiza kazi zake hatachaguliwa tena. Au ataondolewa kabla ya kipindi chake kumalizika. Mkiweza kuwa na serikali ya mtaa inayofanana na serikali kuu mnayoitaka, hapo ndipo mnaweza kuanza kuzungumzia kubadili mfumo wa serikali kuu. Lakini kama mwenyekiti wa mtaa ni mzembe, mwongo, mbadhirifu, na mla rushwa na mnaendelea kumchagua maana anawapa pilau au ni shemeji yako, usitarajie utaweza kuleta mabadiliko huko juu. Kama hamna mbinu za kubadili serikali za mitaa, mtawezaje kubadili serikali kuu? Kwanini unataka serikali kuu yenye dira na kuwajibika ila sio serikali za mitaa yenye kutii wajibu wake wakati ampapo ndio mko nazo karibu? Uko Sumbawanga unataka kumbadili Rais Mkapa wakati mwenyekiti wako wa kijiji ni mlevi wa gongo?
Mwanzo mpya ninaouzungumzia unahitaji kujitoa mhanga kwa kuhoji hata imani zetu. Kuhoji viongozi wa dini zetu. Kwa mfano, kwanini unataka kuwajibisha na kuhoji viongozi wa mambo ya kidunia (yaani wa serikali) lakini sio viongozi wa kidini (mambo ya akhera)? Tazama wanaharakati wa kijinsia wanaounda vyama, mitandao, na kufanya mikutano na makongamano ili kuondoa udhalimu wa mfumo dume. Wanaharakati hawa wanaisukuma sirikali ili iweke mazingira ya kisheria na kisera ambayo yatatoa nafasi sawa kwa wanawake na wanaume katika nyanja za elimu, uongozi, n.k. Wanaharakati hawa wanawashauri, wanawahimiza, na kuwaunga mkono wanawake wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi. Tunawasikia hivi sasa wakishauri taifa letu liwe na rais mwanamke.
Hivi ni kitu gani kinawafanya wanaharakati hawa wagombee haki za wanawake za kisiasa na kiuchumi lakini sio za kidini na kiimani? Wanawezaje kuitaka sirikali kuhakikisha kuwa wanawake wanapewa nafasi sawa katika jamii lakini hawataki dini zao kutoa nafasi hiyo sawa? Unakuwa mwanaharakati wa haki za wanawake na wakati huo huo dini yako hampi mwanamke huyo unayemtetea haki sawa? Kwanini unataka wanawake wawe viongozi kwenye shughuli za siasa, uchumi, na utawala ila sio kwenye dini? Ni lini wanawake watakuwa mapapa na maaskofu? Ni lini wataruhusiwa kuhubiri mbele ya umma wa wakatoliki au waislamu? Ni lini tutawaona wakiwa kwenye uongozi wa juu wa Bakwata au jimbo kuu?
Kama hawana haki au uwezo wa kuwa na uongozi kwenye mambo ya maana kama ya imani, mambo yanayomhusu muumba, kwanini wawe na haki na uwezo wa kuongoza kwenye mambo ya kibinadamu? Kwanini unataka serikali inayoongozwa na wanadamu iwape haki sawa wakati dini inayoongozwa na mungu (kama mnavyodai) haiwapi hizo haki? Kama mungu hapendi wanawake wawe na haki sawa, tukisema kuwa mfumo dume ni mfumo tunaoiga toka kwa mungu tutakuwa tumekosea? Kama mungu hataki wanawake waongoze mambo yake au wahubiri juu yake, kwanini sisi tuwachague watuongoze? Kama mwanamke hawezi kuwa kiongozi wa juu wa wakristo au waislamu, kwanini apewe uongozi wa juu wa nchi? Kama mungu hataki wanawake wawe mashehe, maimamu, mapadri, maaskofu, n.k. kwanini sisi tung'ang'anie kuwa na rais mwanamke?
Haki ya mwanamke inayodaiwa kwenye ulingo wa siasa ni haki hiyo hiyo ambayo inapaswa kudaiwa katika dini zinazoongozwa na wanaume wanaojichukulia kuwa ni bora zaidi. Akisimama shehe au padri kuitaka serikali kujenga demokrasia, mwambie aanze kwanza yeye kwenye imani yake. Mwanaharakati yeyote wa jinsia, awe mwanaume au mwanamke, lazima apambane na mfumo dume ulioundiwa aya za manabii ili kumbagua, kumdhalilisha, na kumkandamiza mwanamke. Ndio kuanza upya huko. Ndio kuvunjavunja kila kitu. Kubomoa na kuanza upya.
ndesanjo macha
|
Shy
Banned
Join Date: Thu Nov 2006
Posts: 4,258
Thanks: 0
Thanked 170 Times in 112 Posts
|
|