Kundi moja linaweza kujitoa na kuunda chama kipya au kujiunga na chama kingine. Hii inaweza kusababisha CCM isiwe na nguvu kama ilivyo sasa na hatimaye kupata Wabunge na Rais ambao watatoka katika chama kingine na kuleta mapinduzi ya kweli Tanzania, badala ya kuendelea na hawa majambazi wanaouza rasilimali za Tanzania kwa wageni na kuendelea kufuja mabilioni ya pesa za walala hoi.
~*~*~*~*~*~*~*~*~*~*~*~*~*~*~* ~*~*~*~*~*~*
CCM yanyemelewa na kashfa ya makundi
na Charles Mullinda
KUNA kila dalili za wazi kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), sasa kinanyemelewa na kashfa nzito ya viongozi wake kutokuwa na maadili mema ya uongozi, ambayo chanzo chake ni makundi yaliyoota mizizi ndani ya chama hicho.
Ingawa hakuna ushahidi wa wazi wa kulithibitisha jambo hilo, ushahidi usio na tone la shaka unaothibitishwa na hali ya mambo inavyoendelea sasa ndani ya chama hicho wakati kikielekea katika uchaguzi wa viongozi wake, unaonyesha hivyo.
Kuibuka kwa kashfa ya ufuska inayomwandama Mbunge wa Viti Maalumu wa chama hicho, Amina Chifupa, ambayo imesababisha atalikiwe na mumewe, Mohamed Mpakanjia, ni mlolongo wa vita ya kuchafuana na kukashifiana, kwa nia ya kuwania madaraka.
Vita hiyo chafu ambayo imekuwa ikiendeshwa na kundi la wanamtandao, sasa inaonekana kushika kasi tena wakati chama hicho kikielekea katika uchaguzi wa viongozi wake, baada ya kutulia kwa muda, ulipomalizika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.
Amina, mmoja wa wabunge vijana wanaoibukia, na mwenye ushawishi katika kundi lake la vijana, anadaiwa kuundiwa kashfa ya kutokuwa mwaminifu katika ndoa yake na kundi la wanamtandao, ambalo limekuwa na sifa ya kuwaengua katika mchuano wa kugombea nafasi za uongozi wale wanaotofautiana na kundi hilo.
Amina, ameingia katika mtego wa wanamtandao baada ya kuonyesha nia ya kugombea nafasi ya juu ya uongozi wa Umoja wa Vijana wa chama hicho, UVCCM, nafasi ambayo inadaiwa kuwa tayari amekwishaandaliwa mtu wa kuirithi na wanamtandao, baada ya mwenyekiti wa sasa wa umoja huo kumaliza muda wake hivi karibuni.
Mwenyewe alikiri hilo mwishoni mwa wiki iliyopita, alipozungumza na vyombo vya habari kuhusu kuvunjika kwa ndoa yake, na kueleza kuwa baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM walikuwa wameamua kwa makusudi kuiharibu ndoa yake ili kupunguza kasi yake ya kuwania uenyekiti wa UVCCM.
Ingawa aliahidi kumtaja mmoja wa viongozi waliohusika na mpango huo, adhima yake hiyo haikufanikiwa baada ya kushindwa kufika Idara ya Habari (MAELEZO) kwa ajili ya kulipua bomu kama alivyopanga, kwa kile kilichoelezwa na baba yake mzazi, Hamis Chifupa, kuwa familia imemkataza.
Hata hivyo, Amina alikaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa kashfa ya ufuska iliyomfanya aachike kwa mumewe iliundwa na mmoja wa viongozi wa juu wa CCM, ambaye pia ni Naibu Waziri na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
Kwamba, mumewe kabla ya kumpa talaka alionekana akitoka ofisini kwa kiongozi huyo wa CCM na serikali, kiongozi ambaye alikwisha kuonyesha nia ya kutomuunga mkono katika azima yake ya kuwania uenyekiti wa UVCCM.
Jambo hilo lilitafsiliwa na Amina mwenyewe pamoja na baadhi ya mashabiki wake kuwa kiongozi huyo ndiye aliyezusha uongo huo, lengo likiwa kumchafua ili ashindwe kutekeleza azima yake.
Mumewe Amina, naye amekwisha kukiri kufika ofisini kwa kada huyo wa CCM muda mfupi kabla ya kwenda kumtaliki mkewe, ingawa hajaweka wazi kitu walichokiongea na kada huyo wa CCM anayedaiwa kuwa mwanamtandao.
Kashfa hii inayodaiwa na Amina kuwa ni ya kuunda, inaingia katika orodha ndefu ya kashfa za aina hii zilizowahi kuwakuta wana CCM wengine waliokuwa wakipambana na kundi la wana mtandao katika chaguzi mbalimbali na kuonekana kuwa tishio.
Tuhuma za ufuska wa Amina zinaingia katika rekodi ndefu ya siasa za kuchafuliana majina zilizoanza kujitokeza waziwazi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, baada ya wagombea waliokuwa wakilipinga kundi la wanamtandao, kuandamwa na kashfa nyingi nzito, ambazo kwa kiasi kikubwa ziliwachafulia majina na kusababisha waonekana kuwa viongozi wasiofaa kushika hatamu za uongozi wa taifa hili.
Miongoni mwa waliokumbwa na makali ya joto la kuundiwa kashfa na kundi la wanamtandao ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu Tatu, Frederick Sumaye, aliyekuwa mmoja wa wagombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2005.
Sumaye alikabiliana na wakati mgumu baada ya kuanza kuandamwa na vyombo vya habari ambavyo wakati akiingia madarakani vilimpamba kama kiongozi mchapakazi, vilipoanza kumshambulia kwa kuanika kashfa mbalimbali zilizodaiwa kufanywa naye, huku ikiwa haifahamiki chanzo cha kashfa hizo.
Kiboko kilichotumiwa na wanamtandao kumpiga Sumaye kilitumiwa pia kumchapa Profesa Mark Mwandosya ambaye alihusishwa na uuzaji mbaya wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), akidaiwa kuhongwa na wawekezaji walionunua kampuni hiyo.
Prof. Mwandosya alijikuta akichafuka vibaya mbele ya macho ya jamii baada ya kudaiwa kuwa kampuni iliyonunua TTCL ilimpa kazi mwanawe wa mwisho, na baadaye akadaiwa kuchangisha fedha za chama huku akiwa si mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Wengine waliokwisha kushughulikiwa na kundi hili la wanamtandao na kuonekana watu wasiofaa kushika nafasi za uongozi walizokuwa wakizitaka ni pamoja na Dk. Salim Ahmed Salim, ambaye alidaiwa kuwa Mwarabu, pamoja na kashfa nyingine nyingi mbaya ambazo ziliharibu kabisa sifa yake ya utumishi uliotukuka kwa taifa hili.
John Samuel Malecela, naye ni muhanga wa vita hii na alijeruhiwa kwa kukashifiwa kwamba Mwalimu Nyerere tangu awali hakumkubali kuwa kiongozi wa juu wa taifa na pia umri nao ulitumiwa kama kigezo cha kummaliza.
Kuibuka kwa vita ya kuchafuana ndani ya CCM kulianza kuonekana katika Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM ambayo ina wanachama wengi katika kundi la wanamtandao, baada ya Mwenyekiti wa sasa wa umoja huo, Dk. Emmanuel Nchimbi, kutofautiana na aliyekuwa Katibu wa Uhamasishaji wa UVCCM, Frank Uhalula.
Mgogoro baina ya viongozi hao wa UVCCM ulimlazimisha Rais Mkapa kuamua kuwatenganisha kwa kuwapangia majukumu makubwa yaliyowafanya wasikae pamoja makao makuu ya umoja huo kwa muda mrefu.
Dk. Nchimbi ambaye alikuwa tayari amekwishamvua madaraka ya Katibu Mhamasishaji, Uhahula, na kuyakabidhi kwa Dk. Diodorus Kamala, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda na Uhahula aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chunya.
Kinachoashilia kuwa baadhi ya viongozi wa chama hicho wanakerwa na tabia hiyo ya kukashifiana ambayo kwa kiasi kikubwa inasababishwa na kuwapo kwa makundi, ni hatua ya hivi karibuni ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula, kumtaka Rais Jakaya Kikwete kuyavunja makundi ndani ya chama hicho.
Follow Us Here